Kila mwaka ifikiapo tarehe 21 mwezi Septemba, Umoja wa Mataifa huadhimisha Siku ya Amani Duniani. Nayo kamati ya Kiekumeni ya Makanisa Duniani imewaomba waumini wote wa makanisa yake kuombea amani siku hiyo.
Baba Mtakatifu baada ya katekesi yake siku ya jumatano kwa halaiki ya waumini na wahujaji waliokusanyika kwenye uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatikani, amewaalika waumini wakatoliki kote ulimwenguni kuungana na wakristo wenzao katika jitihada za kumwomba Mungu kuwajalia zawadi ya amani wote wenye kuishi kwenye maeneo yanayokumbwa na migogoro ya kivita.
Ni ombi la Baba Mtakatifu Francisko kwamba amani itawale kwenye mioyo ya watu wote, na kwamba kila mtu atajitahidi kuwashawishi viongozi wa dunia kutafuta suluhisho la kidiplomasia na kisiasa kwa ajili ya kuleta amani kwenye maeneo ambayo wakazi wake waanaendelea kuteseka kwa ajili ya migogoro.
Ni mazungumzo na majadiliano tu yanayoweza kuleta amani ya kudumu na kuhakikisha kwamba haki na heshima ya kila mwanadamu, na hasa wale walio dhaifu zaidi, inaendelezwa, asema baba Mtakatifu. Chanzo: Radio Vatican Swahili